Nini hutokea baada ya kutumia vidonge vya kutoa mimba?

Baada ya kutumia vidonge vya kutoa mimba, watu wengi hupata maumivu ya tumbo, kutokwa na damu, na madhara kama kichefuchefu au baridi. Haya ni ya kawaida na yanaonyesha kuwa vidonge vinafanya kazi. Matatizo makubwa ni nadra lakini yanaweza kujumuisha kutokwa na damu nyingi, maumivu makali, na homa baada ya saa 24. Sikiliza mwili wako na utafute msaada wa kiafya ukiona dalili za hatari.

Zipo njia mbili za utoaji mimba kwa kutumia vidonge – njia ya kwanza ni kutumia kwa pamoja mifepristone na misoprostol na yapili ni kutumia misoprostol pekee. Njia zote mbili zina ufanisi mkubwa. Matokeo baada ya matumizi ya vidonge hivi vya utoaji mimba hutofautiana kati ya mtu na mtu.

Ni dalili na athari gani za kutumia vidonge vya kutoa mimba?
Nitajuaje kama nina matatizo baada ya kutumia vidonge vya kutoa mimba?
Nitarajie nini ndani ya wiki kadhaa baada ya kutoa mimba?
After Use Pills

Ni dalili na athari gani za kutumia vidonge vya kutoa mimba?

Baada ya kutumia mifepristone

Mifepristone kwa kawaida haina madhara makubwa—unaweza kuendelea na shughuli zako kama kawaida. Baadhi ya watu wanaweza kuhisi kichefuchefu zaidi, uchovu, au kutokwa damu kidogo, lakini ni kawaida pia kutohisi chochote kabisa.

Baada ya kutumia misoprostol

Maumivu ya tumbo na kutokwa damu ni madhara makuu. Dalili hizi ni muhimu kwa sababu zinaonyesha kuwa dawa inafanya kazi. Ni kiasi gani cha maumivu na damu kinachotarajiwa?

Kwa baadhi ya watu, maumivu ya tumbo ni makali – huwa zaidi ya maumivu ya hedhi.

Wakati mwingine, damu inaweza kuwa nyingi kuliko kipindi cha kawaida cha hedhi. Pia ni kawaida kutoa mabonge ya damu saa chache baada ya kutumia misoprostol. Ukubwa wa mabonge ya damu utatofautiana kulingana na umri wa ujauzito. Katika ujauzito wa awali, hata vibonge vidogo vya damu vinaweza kuonesha kuwa mimba imetoka. Baada ya wiki 10, unaweza kuona au kuhisi kiumbe cha mtoto au fetasi inapopita.

Na kwa baadhi ya watu, maumivu ya tumbo ni madogo na damu ni ile ya hedhi ya kawaida. Usijali ikiwa utapata damu na maumivu zaidi kuliko kipindi cha kawaida cha hedhi.

Ikiwa utapata maumivu makali ya tumbo, tumia vidonge vitatu hadi vinne vya ibuprofen (mg 200) kila baada ya saa sita hadi nane. Hii inapaswa kukufanya ujisikie vizuri. Pia unaweza kutumia pedi ya moto, kuoga kwa maji moto, au kunywa chai moto.

Unaweza kunywa na kula chochote unachotaka.

Jaribu kukaa mahali pazuri hadi ujisikie vizuri.

Unapaswa kujisikia vizuri ndani ya masaa 24.

Watu wengine hupata madhara mengine, kama vile:

  • baridi,
  • kizunguzungu,
  • homa,
  • kichefuchefu au kutapika,
  • kuhara, na
  • maumivu ya kichwa.

Ingawa ni ya kusumbua, madhara haya si dalili za hatari. Jaribu kunywa maji mengi na kujihudumia ili uweze kuwa na faraja.

Watu wengi wataacha kuhisi dalili za ujauzito, kama vile kichefuchefu, ndani ya siku chache. Maumivu ya matiti mara nyingi ndiyo dalili ya mwisho kupotea na dalili hii inaweza kudumu hadi siku 10 baada ya kutumia misoprostol.

Kumbuka:

Ni bora kufanya kipimo cha ujauzito wiki nne hadi tano baada ya kutoa mimba, ili kuhakikisha endapo ilitoka au la. Waweza tumia kipimo cha mkojo au damu. Ikiwa utafanya kipimo mapema, waweza kupata matokeo yasiyo sahihi yanayo onesha kuwa bado una ujauzito. Hata hivyo, sikiliza mwili wako; ikiwa utaendelea kuhisi dalili za ujauzito (maumivu ya matiti, kichefuchefu, uchovu, n.k.) baada ya kutumia vidonge, nivyema kufanya uchunguzi wa ultrasound ili kuthibitisha kama mimba ilitoka au la.

Nitajuaje kama nina matatizo baada ya kutumia vidonge vya kutoa mimba?

Wakati wa kutoa mimba, dalili zilizo orodheshwa hapo juu ni za kawaida na matatizo hutokea kwa nadra sana. Zifuatazo zinaweza kuwa ishara za hatari. Kuwa makini.

Kutokwa na damu nyingi

Ikiwa utajaza pedi mbili za kawaida, ndani ya saa moja na hali hiyo ikaendelea kwa saa mbili mfululizo baada ya kutoa mimba, hii inachukuliwa kama damu ya ziada. Unapaswa kutafuta msaada wa matibabu ikiwa damu itatoka kwa namna hii. Kujaza kunako zungumziwa hapa humaanisha kwamba pedi imeshiba kabisa damu, kutoka mbele hadi nyuma, kutoka upande mmoja hadi mwingine, na kila mahali.

Maumivu makali

Ikiwa una maumivu makali ambayo hayapungui hata baada ya kutumia ibuprofen, tafuta msaada wa matibabu. Aina hii ya maumivu makali inaweza kumaanisha kuwa una tatizo linalohusiana na ujauzito wako. Maumivu yasiyoisha na ambayo hayapunguzwi na ibuprofen yanaweza kuwa ishara ya hatari. Katika hali kama hizi, tunapendekeza utafute huduma za afya.

Kuhisi mgonjwa sana

Unaweza kuwa na homa au kuhisi kichefuchefu na kutapika siku unapotumia misoprostol. Hili ni jambo la kawaida, lakini unapaswa kupata nafuu zaidi siku inayofuata. Ikiwa utaanza kuhisi vibaya zaidi, tafuta msaada wa matibabu.

Kutokwa na uchafu wenye harufu mbaya ukeni

Damu yako inaweza kuwa na harufu mbaya kidogo na inaweza kuwa nyekundu iliyokolea, nyekundu angavu, au kahawia, lakini ikiwa uchafu una rangi tofauti na unanuka vibaya kama umeoza, inaweza kuwa ishara ya maambukizi.

Homa ya kudumu

Ikiwa unapata homa ya 38°C (100.4°F) inayojitokeza angalau saa 24 baada ya kutumia misoprostol na haishuki baada ya kutumia ibuprofen, unapaswa kutafuta msaada wa matibabu.

Madhara ya mzio.

Ikiwa utapata madhara ya mzio (kama vile mikono kuwasha, wekundu au uvimbe kwenye uso au shingo), unaweza kutumia dawa ya kupambana na mzio au antihistamine. Hata hivyo, ikiwa utapata ugumu wa kupumua, inamaanisha kuwa ni mzio mkubwa sana na unahitaji msaada wa matibabu haraka.

Nitarajie nini ndani ya wiki kadhaa baada ya kutoa mimba?

Jambo muhimu zaidi ni kusikiliza mwili wako. Unaweza kujihisi uchovu kidogo; pumzika wakati wowote unapohitaji.

Tumia pedi kufuatilia utokaji wako wa damu. pindi utakapo jiridhisha kuwa kila kitu kipo sawa, waweza kutumia tamponi au kikombe.

Unaweza kuendelea na shughuli zako za kawaida pindi utakapo ona uko tayari. Hii inategemea na wewe mwenyewe.

Ni salama kufanya ngono unapohisi uko tayari, lakini kumbuka kuwa unaweza kushika ujauzito tena ndani ya wiki mbili baada ya kutoa ujauzito, hata kama bado unatokwa na damu.

Ni kawaida kuhisi hisia tofauti. Baadhi ya watu hujihisi vizuri mara moja, huku wengine wakihitaji muda zaidi. Kuzungumza na mtu unayemwamini kunaweza kusaidia. Pia, unaweza kuwasiliana na marafiki zetu kupitia safe2choose.org.

Waandishi:

Yote yaliyomo kwenye wavuti hii yameandikwa na timu ya HowToUseAbortionPill.org kwa kufuata viwango na itifaki kutoka Shirikisho la Kitaifa la Utoaji Mimba, Ipas, Shirika la Afya Ulimwenguni, DKT Kimataifa na carafem.

Marejeo: